AMKA NA BWANA

                   SOMO LA ASUBUHI
                    KESHA LA ASUBUHI

JUMANNE-AGOSTI 22, 2017

UPONYAJI WA KIMBINGU

"Nakusihi, Bwana, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana." 2 Wafalme 20:3.

▶Katikati ya utawala wenye mafanikio, Mfalme Hezekia alipatwa na ugonjwa wa kutisha kwa ghafla. “Akaugua,…akawa katika hatari ya kufa,” hakuna mtu ambaye angeweza kumsaidia. Tumaini kidogo lililokuwa limesalia, lilionekana kuondolewa wakati nabii Isaya alipotokea mbele yake akiwa na ujumbe huu, “Bwana asema hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.”

▶Hali ilionekana kutokuwa na tumaini kabisa; hata hivyo bado mfalme aliweza kumwomba Yeye ambaye tangu mwanzo alikuwa ndiye kwake “kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso” (Zaburi 46:1). Hivyo, “akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana.”…

▶Yeye ambaye “rehema zake hazikomi,” alisikia sala ya mtumishi wake. “Ikawa, kabla Isaya hajatoka katika mji wa kati, neno la Bwana likamjia, kusema, Rudi, ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wangu, Bwana, Mungu wa Daudi baba yako asema hivi, Nimeyasikia maombi yako, na kuyaona machozi yako; tazama, nitakuponya….” Kwa furaha nabii alirudi akiwa na maneno ya imani na tumaini. Huku akielekeza kwamba bonge la mkate wa tini liwekwe katika sehemu iliyo na ugonjwa, Isaya aliwasilisha kwa mfalme ujumbe wa rehema ya Mungu na uangalizi wake unaolinda.

▶Wale wanahitaji kuponywa kwa maombi haipasi wapuuzie matumizi ya njia za tiba zinazopatikana. Matumizi ya tiba hizo kama ambavyo Mungu amezitoa ili kupunguza maumivu na kusaidia uumbaji asili katika kazi yake ya urejeshwaji, hayamaanishi kuikana imani….

▶Mungu ametupa uwezo wa kupata ujuzi wa kanuni za uhai. Ujuzi huu umewekwa pale tulipo ili tuutumie. Inatupasa tutumie kila nyenzo kwa ajili ya urejeshwaji wa afya, tukichukua kila fursa inayowezekana, tukitenda hivyo katika upatanifu na kanuni za asili. Tunapokuwa tumeomba kwa ajili ya uponywaji wa mgonjwa, tunaweza kufanya kazi kwa nguvu zaidi, tukimshukuru Mungu kwamba tunayo fadhila ya kushirikiana naye na kuomba baraka yake katika vile vitu ambavyo yeye mwenyewe amevitoa.

Maoni

Machapisho Maarufu